Header Ads

DIAMOND ALIAMBIWA SIMU ANAZO SHILOLE

Stori:Shakoor Jongo na Musa Mateja
STAA wa filamu na muziki wa Bongo Fleva, Zuwena Mohammed ‘Shilole’ ameingia matatani akidaiwa kuingia mitini na simu tatu za mkononi alizoaminiwa nchini Afrika ya Kusini alikokwenda kufanya shoo.
Msanii huyo alikumbwa na kasheshe hilo Julai 19, 2013 nyumbani kwa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’, Sinza Mori, Dar.
Siku hiyo Diamond alikuwa akifuturisha na aliwaalika watu mbalimbali wakiwemo mastaa lakini nusura futuru iingie doa kufuatia zogo hilo.

ISHU ILIKUWAJE?
Ndugu wa Diamond aitwaye Majaliwa Majuto ‘Q Boy’ alidai ndiye mwenye simu hizo. Alisema miezi kadhaa iliyopita, Shilole alikwenda nchini humo kufanya shoo ya muziki. Wakati wa kuondoka alimpa simu tatu, Ipad, Samsung Galaxy na Blackberry ili akifika Bongo ampe Diamond lakini msanii huyo hakufanya hivyo.

“Alikuja Sauzi kufanya shoo, wakati wa kuondoka nilimpa simu tatu amletee Diamond lakini nashangaa hakufanya hivyo na mimi tangu nirudi Bongo simpati, kila nikimpigia simu hapokei, leo ndiyo tumekutana hapa kwa Diamond,” alilalama Q Boy.
DIAMOND ALIAMBIWA SIMU ANAZO SHILOLE
Alisema awali akiwa nchini humo baada ya kumkabidhi mali hizo, alimpigia simu Diamond na kumtaarifu kuwa ‘mzigo’ anao Shilole, akashangaa staa huyo kujibu kwamba hajazipata wala hajamwona Shilole.

SHILOLE AJITETEA
Katikati ya mzozo huo, Shilole alijitetea kwa kusema: Mi namdai rafiki yake fedha yangu ya shoo iliyobaki, kama shilingi laki nane hivi ndiyo maana nikaamua kuzizuia simu za huyu (Q Boy) hadi nimaliziwe pesa yangu.
Hata hivyo, katika sakata hilo ilielezwa kuwa Shilole na Q Boy hawakuwa na makubaliano yoyote kuhusu shoo hiyo na simu hizo hivyo madai ya mwigizaji huyo ni ‘usanii’ tu.

MAMA DIAMOND AINGILIA KATI KUOKOA
Zogo hilo lilipopamba moto na kuashiria kuvurugika kwa amani, mama mzazi wa Diamond, Sanura Kasim ‘Sandra’ aliamua kuingilia kati na kuagiza suala la kudaiana simu lifanyike kesho yake (Jumamosi) kwa vile siku hiyo haikuwa muafaka.
“Jamani! Jamani! We nani, Shilole na we Majaliwa, naomba kwa leo muepusheni shetani kwani hapa si mahali pake, ila kesho tutaitana na kumaliza suala hili, mimi mwenyewe nitalisimamia,” alisema bi mkubwa huyo na kumaliza henyahenya iliyoibuka.

No comments